WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Masanja Kadogosa, kutayarisha timu ya vijana kuwafundisha kwa ajili ya kuhudumia reli ya kisasa ya Standard Gauge (SGR) itakapokamilika.
Profesa Mabarawa alitoa agizo hilo jana wakati alipotembelea mradi huo kutoka Soga Kibaha mkoani Pwani hadi Pugu jijini Dar es Salaam, ili kujionea maendeleo ya mradi huo unaotarajiwa kukamilika Juni 2020 na kwa awamu ya kwanza ikiwa imeanzwa kutekelezwa kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro kwa urefu wa kilometa 300.
Alisema suala la kuwafundisha vijana kwa ajili ya kuhudumia reli hiyo lipo kwenye mkataba kati ya Rahco na Kampuni ya Yapi Merkezi ya Uturuki inayojenga reli hiyo hivyo ni vyema wakaandaa vijana sasa kwa ajili ya kuwapeleka kwenye mafunzo ili reli hiyo itakapoanza kazi iendeshwe na Watanzania.
“Hii treni inajengwa leo baada ya miaka miwili itakuwa imekamilika, treni hii ni ya umeme kila kitu hapa kitakuwa cha kisasa kama vijana hatukuwapeleka leo kwenda kujifunza tutakuwa tumejenga treni ya kisasa, lakini haina watu wa kuendesha na sisi hatutaki iwe hivyo, tunataka tuone Watanzania waendeshaji wa treni, mafundi wa sehemu mbalimbali ili kuhakikisha mradi huu wa Watanzania unaendeshwa na Watanzania,” alisema Mbarawa.
Alisema mradi huo kwa sasa umekamilika kwa asilimia 5.86 badala ya asilimia 6.8 kama ilivyotakiwa, na hiyo imetokana na mvua zilizonyesha na kusababisha ujenzi huo kushindwa kukamilika kama ilivyotakiwa.
“Kuna tofauti ya asilimia moja na imetokana na hali ya mvua, lakini sasa wamejipanga upya kuhakikisha kwamba wanaongeza watu na vifaa ili kuhakikisha kama tulivyopanga ifikapo Juni 2020, reli hii Watanzania iwe imemalizika na kuanza kutumika,” aliongeza.
Alieleza kuwa kazi inayoendelea sasa ni kukata maeneo, kujaza na kuweka sawa kwa ajili ya kutandika reli na wataanza kujenga madaraja katika eneo la Pugu.
No comments:
Post a Comment