Rais wa Marekani Donald Trump amemjibu Jay-Z baada ya mwanamuziki huyo wa muziki wa Rap kumuita "mdudu hatari'' na kumkaripia kwa namna anavyowachukulia watu weusi.
Katika ujumbe kwenye Twitter Bw Trump alisema kuwa "kiwango cha Wamarekani wasio na ajira kimeripotiwa kuwa cha chini kabisa kuwahi kurekodiwa!" kwa sababu ya sera zake.
WaMarekani wenye asili ya Afrika wasio na ajira ni asilimia 6.8%, kiwango ambacho ni cha chini kuwahi zaidi kurekodiwa.
Lakini wakosoaji wanasema kuwa kiwango cha ukuaji wa uchumi kilianza kuimarika wakati wa rais Obama na kwamba ukosefu wa ajira miongoni mwa watu weusi umesalia kuwa wa kiwango cha juu miongoni mwao kuliko miongoni mwa wazungu.
Alipokuwa katika kipindi cha televisheni ya CNN cha Van Jones Show, Jay-Z alisema kuwa kuangazia viwango vya ukosefu wa ajira ni " kukosa ufahamu wa mambo".
"Sio suala la ukosefu wa pesa pekee lenye umuhimu … pesa hazileti furaha... hazileti. Hii ni kushindwa kuelewa ukweli. Uwachukulie watu kama binadamu ...hilo ndio suala kuu la muhimu."
Aidha amesema kuwa kuchaguliwa kwa Bw Trump kulitokana na kushindwa kutatuliwa kikamilifu kwa masuala kadhaa."Umepuliza manukato katika debe la taka," alisema. "Unapofanya hivyo ni kwamba unawafanya wadudu hatari kufika. Unapopuliza kitu basi unasababisha kuzaliwa kwa wadudu hatari kwa sababu haungazii tatizo halisi."
"Hauchukui taka nje, unaendelea kupuliza dawa juu yake ili kulifanya debe la taka kukubalika. Vitu hivyo vinapokuwa, huwa unabuni mdudu hatari . Na kwa sasa mdudu hatari tuliyr naye ni Donald Trump, mdudu hatari."
Jay-Z alimuunga mkono Barack Obama wakati wa uongozi wake, na alimsifia Bi Hillary Clinton katika uchaguzi wa mwaka 2016 ambapo Bwana Trump alishinda
Pia aliulizwa kuhusu madai ya rais Trump kuyataja mataifa ya Afrika kuwa "machafu" au mataifa ya "mabwege"
Hatua hiyo ilimfanya kushutumiwa vikali na viongozi wa AU na baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika kama vile Botswana na Ghana.
Bw Trump amekanusha kwamba alitumia neno hilo kuyaelezea mataifa ya Afrika.
Hata hivyo alikiri kwamba alitumia maneno makali akiyaeleza mataifa ya Afrika, Haiti na El Salvador alipokuwa anazungumzia wahamiaji wanaoingia Marekani.
"Inasikitisha na inaumiza," alisema Jay-Z. "Kila mtu anahisi hasira. Baada ya hasira, inasikitisha sana kwa sababu ni kama ana dharau kwa watu wote ."
Rais Trump amekanusha madai yote kwamba ya ubaguzi dhidi yake.
Alisema kuwa lugha aliyoitumia ilikuwa ni ya ''ukali '' lakini anakana kutumia neno linaloripotiwa.
No comments:
Post a Comment