Tido Mhando kizimbani kwa uhujumu uchumi - HabariMagic

Breaking

Kerajaan

BANNER 728X90

Saturday, January 27, 2018

Tido Mhando kizimbani kwa uhujumu uchumi

ALIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando akiwa mahakamani.
LIYEKUWA Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando amefi kishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka ya uhujumu uchumi kwa kuisababishia serikali hasara ya Sh milioni 887.1.
Tido ambaye sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Azam Media, alifi kishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kusomewa mashtaka matano mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa.
Akisoma mashitaka hayo katika Kesi ya Uhujumu Uchumi Namba 7/2018, Mwendesha Mashitaka wa Takukuru, Leonard Swai alidai kuwa Juni 16, 2008 maeneo ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Dubai, akiwa mtumishi wa umma kama Mkurugenzi Mkuu wa TBC, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kuendesha programu za utangazaji kati ya TBC na Shirika la Channel 2 Group (BVI) bila ya kutangaza zabuni.
Swai alidai kuwa kitendo hicho ni kinyume cha Kifungu Namba 31 cha Sheria ya Manunuzi na Ugavi Namba 21 ya mwaka 2004, ambapo alisababisha Shirika la Channel 2 Group kupata faida.
Katika mashitaka ya pili, ilidaiwa Juni 20, 2008 katika nchi za Kiarabu, Dubai, akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kuingia mkataba wa Digital Terrestrial Broadcasting kati ya TBC na Channel 2 Group bila kutangaza zabuni, kinyume cha sheria na kusababisha shirika hilo kupata faida.
Pia ilidaiwa kati ya Agosti 11, 2008 na Septemba 4, 2008 maeneo ya nchi za Kiarabu, Dubai akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa kununua, kusambaza na kusimika vifaa na minara ya utangazaji kati ya TBC na BVI bila kutangaza zabuni, kinyume cha Sheria ya Manunuzi na Ugavi na kusababisha BVI kupata faida.
Katika mashitaka ya nne, ilidaiwa kuwa Novemba 16, 2008 nchini Dubai, akiwa mtumishi wa umma na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Tido alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini mkataba wa DTT Broadcast Infrastructure kati ya TBC na BVI bila kutangaza zabuni, kinyume cha sheria na kusababisha shirika hilo kupata faida.
Akisoma mashitaka ya tano, Wakili Dismas Muganyizi alidai kati ya Juni 16, 2008 na Novemba 1, 2008, Dubai akiwa Mkurugenzi Mkuu wa TBC alitumia madaraka yake vibaya na kusababisha TBC kupata hasara la Sh milioni 887.1. Mshitakiwa alikana mashitaka hayo.
Swai alidai upelelezi wa shauri hilo umekamilika na kwamba wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshitakiwa maelezo ya awali. Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Mathayo Maleta alidai kuwa mteja wake amekana mashtaka anaomba dhamana.
Hakimu Nongwa aliyataja masharti ya dhamana kuwa atatakiwa kutoa fedha taslimu ya nusu aliyosababisha hasara ambayo ni Sh milioni 444 au hati ya mali isiyohamishika yenye gharama hiyo.
Pia alimtaka kuwa na wadhamini wawili wenye anuani za kuaminika watakaosaini dhamana ya Sh milioni 500 na kwamba mshitakiwa hatatakiwa kutoka nje ya nchi bila ya kibali cha mahakama.
Mshitakiwa alitimiza masharti na kuachiwa kwa dhamana na kesi imeahirishwa hadi Februari 23, mwaka huu kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali. Tido aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Mwananchi Communication Limited mwaka 2012 baada ya kutoka TBC na kabla ya hapo, alikuwa Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kati ya 1999 hadi 2006 alipostaafu kazi hiyo jijini London nchini Uingereza.

No comments:

Post a Comment