MELI mbili za mizigo za MV Njombe na MV Ruvuma ambazo zinasimamiwa na kuendeshwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), zimezidi kupasua anga nchini Malawi.
Wafanyabishara kadhaa wa nchini Malawi wamevutiwa na huduma zitolewazo na meli hizo na sasa wamejipanga kusafirisha shehena kubwa zaidi ya mizigo kati ya Tanzania na Malawi.
Moja kati ya kampuni hizo za Malawi ni pamoja na Kampuni ya Farmers World Ltd ambayo ndiyo iliyosafirisha shehena hiyo ya kwanza ya saruji kwenda nchini Malawi. Mdhibiti Mkuu wa Fedha wa kampuni hiyo, Johann Synders amesema wamefurahishwa na huduma waliyopata katika meli hiyo na ameahidi kuendelea kusafirisha shehena nyingine zaidi.
“Nimefurahishwa na jinsi TPA ilivyosafirisha shehena yetu ya saruji kwani imefika ikiwa salama na kwa gharama nafuu ukilinganisha na barabara ambayo imekuwa gharama sana kwa upande wetu,” alisema Synders.
Synders alisema wanafanya tathmini ya gharama ili watumie meli hizo kusafirishia mbolea kutoka Dar es Salaam kupitia Bandari ya Kyela na Nkhata Bay kwa upande wa Malawi kwani itakuwa nafuu kwa kwa biashara yao.
Meli hizo ambazo zina uwezo wa kubeba mzigo wenye uzito wa tani 1,000 kila moja, zimeshaanza safari za kwenda Malawi, ambako MV Njombe imesafirisha jumla ya tani 800 za saruji hadi bandari ya Nkhata Bay nchini humo.
Wakati MV Njombe ikisafirisha shehena hiyo ya saruji, meli nyingine ya mizigo ya MV Ruvuma nayo ipo njiani kwenda bandari ya Monkey Bay, Malawi na shehena ya tani 800 za ‘clinker’.
‘Clinker’ ni malighafi inayotumika kuzalisha saruji, kuisafirisha kwake nchi za nje ni sehemu ya serikali kupata mapato hususan fedha za kigeni. Kampuni hiyo ambayo imesafirisha jumla ya tani 800 za saruji nchini Malawi, ndiyo kampuni kubwa zaidi nchini humo ambayo hujihusisha na biashara ya kuuza bidhaa mbalimbali.
No comments:
Post a Comment