Uchumi Tanzania wagusa wananchi - HabariMagic

Breaking

Kerajaan

BANNER 728X90

Saturday, January 27, 2018

Uchumi Tanzania wagusa wananchi

USIMAMIZI mzuri na utekelezaji wa sera mbalimbali za kuwawezesha wananchi kushiriki kikamilifu kujenga na kumiliki uchumi, kumeifanya Tanzania kuibuka kinara miongoni mwa nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kuwa na Uchumi Jumuishi unaokua duniani.
Taarifa iliyotolewa na Word Economic Forum (WEF) kupitia mradi wake wa ‘The Inclusive Development Index’, imeitaja Tanzania kushika nafasi ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya 48 kati ya nchi 103 zilizofanyiwa tathmini ya nchi zenye Uchumi Jumuishi duniani.
Katika orodha ya nchi 10 bora, nchi zilizofuatia za Afrika na nafasi ziliyoshika kidunia ni Ghana (52), Cameron (53), Burundi (55), Namibia (56), Rwanda (57), Uganda (59), Mali (60), Senegal (61) na Nigeria (63).
Takwimu za ukuaji huu zinaakisi moja kwa moja kauli ya Rais John Magufuli ambaye amekuwa akielezea kutaka uchumi wa Tanzania umilikiwe na wananchi kwa njia mbalimbali ikiwemo kutekeleza sera ya uchumi wa viwanda ambao Watanzania wengi hivi sasa wamekuwa wakitekeleza sera hiyo kwa kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo.
Mtaalamu mbobevu wa masuala ya uchumi na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi, ameeleza kuwa takwimu zilizotolewa na taasisi hiyo zinatafsiri kuwa uchumi wa Tanzania unaelekea kumilikiwa na watu wengi zaidi jambo ambalo litasaidia kupunguza pengo la kipato kati ya walionacho na wasionacho.
Profesa Ngowi ameeleza kuwa uchumi wa aina hiyo unawashirikisha wananchi kumiliki uchumi na kuwafanya watu wengi kufaidi matunda ya ukuaji wa uchumi wa nchi. “Taarifa hizi ni njema kwani kitaalamu tunaita ‘broad based economy’ ambapo watu wengi wanashirikishwa kumiliki uchumi na wengi wanafaidi,” alieleza Profesa Ngowi na kuongeza kuwa kuna nchi zingine zinauchumi mzuri, lakini unamilikiwa na watu wachache na kufanya kuwa na pengo kubwa kati ya walionacho na wasionacho.
Katika siku za hivi karibuni, taasisi mbalimbali duniani ikiwemo Shirika la Fedha Duniani (IMF), Benki ya Dunia (WB) na Taasisi ya Goldman Sachs ya Marekani zimekuwa zikitoa ripoti zikiielezea Tanzania kupaa kiuchumi.
Taasisi hizo zilitabiri kuwa, wakati uchumi wa dunia utakua kwa wastani wa asilimia 3.0 hadi 4.0, ukuaji wa uchumi wa Tanzania unatajwa kuendelea kuwa kati ya nchi tano bora za Afrika ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.5 hadi 7.0 katika mwaka 2018

No comments:

Post a Comment