MAKONDA:Ukijifungua siku ya pasaka uje uchukue zawadi - HabariMagic

Breaking

Kerajaan

BANNER 728X90

Thursday, March 29, 2018

MAKONDA:Ukijifungua siku ya pasaka uje uchukue zawadi

KATIKA kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa zawadi ya vifaa tiba vya kujifungulia 200 vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 20 kwa kina mama watakaojifungua kipindi hiki cha Pasaka.
Vifaa hivyo vitasambazwa katika Manispaa tano za mkoa huo ambazo zitapelekwa kwenye vituo vya afya vilivyopo katika Manispaa hizo huku kila halmashauri ikipata maboksi manne yenye mifuko 40. Akikabidhi vifaa hivyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dk Grace Maghembe alisema Makonda ametoa msaada kama zawadi ya Sikukuu ya Pasaka baada ya kubaini changamoto ya baadhi ya kinamama kushindwa kumudu gharama ya vifaa vya kujifungulia na kujikuta wanatumia kanga au nguo jambo ambalo ni hatari kiafya kwa mama na mtoto.
Alisema gharama ya jozi moja ya vifaa hivyo vya kisasa inakadiriwa kuwa ni Sh 100,000 jambo ambalo kina mama wengi wanashindwa kumudu. Alisema katika kila mfuko mmoja kutakuwa na karatasi maalumu la kujifungulia, blanketi la mtoto, dawa, mabomba ya sindano, pamba, kibanio cha kitovu, nyuzi, pedi za kinamama, dawa ya kuzuia upotevu wa damu, nyembe na glovu ambapo vitatolewa bure kwa kina mama wote watakaojifungua msimu wa Pasaka.

Akitaja vituo vya afya vitakavyonufaika na zawadi hizo kwa kila Manispaa alisema Manispaa ya Kinondoni Kituo cha Afya Tandale, Tegeta, Bunju na Kunduchi na Manispaa ya Ilala Kituo cha Afya Kinyerezi, Pugu, Kitunda na Buguruni. Kwa Manispaa ya Kigamboni ni Kituo cha Afya Kigamboni, Vijibweni, Mjimwema, na Kibada na Manispaa ya Temeke kituo cha afya Yombo Vituka, Roundtable Mbagala, Chamazi na Majimatitu na Manispaa ya Ubungo kituo cha Kimara, Mbezi, Makurumla pamoja na Goba. Aidha Maghembe aliwataka wasimamizi wa vituo hivyo kuhakikisha wanatumia vifaa hivyo kama ilivyokusudiwa na kusema kuwa vitasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.

No comments:

Post a Comment